LUIS Figo ambaye amejidhatiti kumng’oa Sepp Blatter kwenye kiti cha urais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), amezindua kampeni zake huku pia akilenga kuongeza idadi ya timu kwenye fainali za Kombe la Dunia kufikia 40 au 48 endapo atashinda uchaguzi wa Mei, uamuzi unaoweza kuinufaisha zaidi Afrika.
Gwiji hilo la soka la Ureno ni mmoja wa wagombea watatu watakaochuana na Blatter katika uchaguzi huo na amesisitiza chini ya uongozi wake, atahakikisha Fifa inazihusisha kwa karibu pia nchi zisizo za Ulaya.
Katika uzinduzi huo wa jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Wembley, Figo alisema: “Naamini tutaangalia uwezekano wa kupanua wigo wa fainali za Kombe la Dunia kutoka timu 32 za mfumo wa sasa hadi kufikia ule wa timu 40 au hata 48.
“Haya yanawezekana kwani si mbaya muda wa michuano ukiongezeka kwa siku tatu mpaka nne. Kama nyongeza hiyo itakuwapo, hakika timu zitakazochukuliwa zitakuwa za kutoka nje ya Ulaya.”
Katika uchaguzi huo wa Mei 29, Figo atavaana na Blatter, Michael van Praag na Prince Ali Bin Al-Hussein. Mgombea huyo mwenye umri wa miaka 42, pia amepanga kuongeza mafungu ya fedha za Fifa kwa mashirikisho ya nchi wanachama kama atashinda uchaguzi huo.
“Fifa inawajibika kwa mashirikisho ya nchi wanachama. Mpango ni kuwa kiasi cha Dola 8 na 10 milioni kitawanywe kwa kila shirikisho mwanachama katika kipindi cha miaka minne,” alisema.
Staa huyo wa zamani wa Real Madrid, pia alizungumzia mambo mengine kadhaa kwenye kampeni zake likiwamo suala la matumizi ya teknolojia kwenye soka ikiwamo ya kuamua kama mpira umevuka mstari wa goli au la.
No comments:
Post a Comment