STRAIKA wa TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Samatta, amesema anatafakari cha kufanya na wenzake aliocheza nao soka la ututoni na kuishi nao pamoja miaka ya nyuma kwao Mbagala, Dar es Salaam.
Samatta aliliambia Mwanaspoti anakumbuka mambo mengi ya mtaani kwani kamwe hawezi kuwatosa rafiki na watu aliokuwa anashirikiana nao akiwa katika harakati za soka mwanzoni.
“Nakumbuka zaidi mambo ya Mbagala, unajua Mbagala ni kwetu, nina mengi ya kukumbuka kuanzia enzi za utotoni wakati wa chandimu, hadi kwenye ndondo na mengine ya mtaani, ’’ alisema.
“Unajua kuna wakati hata nikiwa Congo nakumbuka mambo ya Mbagala ndiyo maana nafikiria kitu cha kufanya kitakachoniweka pamoja na wenzangu wa zamani, majirani na marafiki.
“Kuna wakati nakuwa na hamu ya hata ya kucheza ndondo, unajua kuna ushabiki fulani ninaoukumbuka, lakini siruhusiwi kufanya hivyo na Mazembe, inaniuma sana hali hii na nikikiuka makubaliano haitakuwa vizuri kwangu labda iwe mechi ya siri lakini hilo haliwezekani.’’
Samatta hakueleweka vizuri kuhusu kutopatikana nyumbani kwao alipokuwa mapumzikoni na kuhusu hilo alijitetea kuwa ni tatizo la uchache wa muda.
“Nakuwa na muda mfupi, na nalazimika kukaa mahali kwa muda mfupi lakini watu wanatoa tafsiri ya mimi kukimbia, kwa mtu asiyejua ratiba yangu vizuri anaweza kuona nawakimbia watu wangu si hivyo kwani hata mimi nakosa mambo mengi kutoka kwao,” alisema.
No comments:
Post a Comment