PLUIJUM AIPA PRESHA AZAM - TodayNews

Tuesday, 5 June 2018

PLUIJUM AIPA PRESHA AZAM




UONGOZI wa Azam FC, umeeleza wazi kuwa wanasajili kutokana na mapendekezo ya kocha wao mpya, Hans Van Der Pluijm, lakini wamekuwa na changamoto kubwa kuhakikisha wanatekeleza matakwa yake.

Tayari Azam imeshawasajili wachezaji wawili ambao ni Donald Ngoma, Tafadzwa Kutinyu, huku kukiwa na tetesi kuwa wanawafukuzia wachezaji wa Yanga, Juma Abdul, Obrey Chirwa na Shafiq Batambuze na mchezaji waliomtoa kwa mkopo Singida, Mudathir Yahya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika makao makuu ya klabu, Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, alisema wamekuwa na mtihani wa kupata wachezaji wanaotakiwa na kocha huyo kwa sababu wengi wanatokea timu kubwa.

Alisema kinachowapa changamoto ni kutokana na wengine kuwa na mikataba, hivyo inakuwa ngumu kuwatoa kwenye timu zao kwa kuvunja mikataba, lakini watahakikisha wanapatikana.


“Usajili unaendelea, tunachokifanya ni kufuata mapendekezo ya mwalimu Hans (Pluijm), kabla ya kusaini naye mkataba, alishatupa kile anachotaka kifanyike, kuhusu wachezaji watakaoachwa, atachagua mwenyewe baada ya kukiona kikosi,” alisema Idd.

Pluijm ambaye awali alikuwa kocha wa Singida United, anajiunga na Azam kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Wakati huo huo, Idd alisema mkataba wa mchezaji wao mpya, Kutinyu, utaongezwa kulingana na kiwango atakachokionyesha.

Alisema mchezaji huyo amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa ya Zimbabwe, inayotarajia kushiriki michuano ya Cosafa na ataanza kuonekana katika kikosi cha Azam kwenye michuano ya Challenji itakayofanyika mwezi ujao.


No comments:

Post a Comment